Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji haramu wa binadamu ni uhalifu wa unyonyaji- UNODC

Usafirishaji haramu wa binadamu ni uhalifu wa unyonyaji- UNODC

Usafirishaji haramu wa binadamu umetajwa kuwa uhalifu wa unyonyaji unaotegemea unyonge, kunawiri penye sintofahamu, na kufaidi pasipo hatua za kukabiliana nao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu dawa za kulevya na uhalifu (UNODC), Yury Fedotov, kuelekea Siku ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu duniani, ambayo huadhimishwa mnamo Julai 30.

Bwana Fedotov amesema wakati jamii ya kimataifa ikipambana na kile kilichotajwa na Katibu Mkuu Ban Ki-moon kuwa mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi na wahamiaji tangu vita vikuu vya pili vya dunia, wasafirishaji haramu wa binadamu na walanguzi wa wahamiaji wanaigeuza taabu ya watu kuwa fursa ya kujinufaisha.

Ameongeza kuwa migogoro na mizozo ya kibinadamu huwaweka watu waliojikuta katikati ya mapigano katika hatari kubwa zaidi ya kusafirishwa kiharamu kwa ajili ya kunyanyaswa kingono, kuondolewa viungo vya mwili, ajira za lazima, utumwa, na aina nyingine za unyanyasaji.