Migogoro ya muda mrefu inaongeza baa la njaa:WFP/FAO

Migogoro ya muda mrefu inaongeza baa la njaa:WFP/FAO

Migogoro ya muda mrefu inayoathiri nchi 17 imewasababisha mamilioni ya watu kutumbukia katika hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula , na kuwa kigingi kwa juhudi za kimataifa za kutokomeza utapia mlo. Hayo yamesemwa leo na mashirika mawili ya Umoja wa mataifa , yakionya katika ripoti yao iliyowasilishwa kwenye baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Mashirika hayo, lile la chakula na kilimo FAO na la mpango wa chakula duniani WFP, yameaandaa taarifa ya mataifa hayo 17 na kuchapisha matokeo yake ambayo yanasema , migogoro sasa imewangiza watu milioni 56 ama katika janga au dharura ya hali ya juu ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

Nchi zinazoongoza orodha hiyo kwa kuwa na watu wengi walioathirika na uhakika wa chakula ni Yemen ambako watu milioni 14 , ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote wan chi hiyo sasa wanakabiliwa na njaa, ikifuatiwa na Syria ambako watu milioni 8.7 sawa na asilimia 37 idadi ya watu wote kabla ya vita, wanahitaji msaada wa haraka wa chakula , lishe na wa kujikimu kimaisha.