Ban ahutubia IGAD kuhusu mzozo wa Sudan Kusini

16 Julai 2016

Ban amesema hayo mjini Kigali Rwanda, wakati akihutubia mkutano wa IGAD, ambapo amewashukuru viongozi wa IGAD kwa juhudi zao katika kuushughulikia mzozo wa Sudan Kusini, akiongeza kuwa isikubalike tena Sudan Kusini kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ban ambaye amesema hakupanga kuwa mjini Kigali, amesema kila mtu ameshangazwa na viwango vya machafuko na ukatili, ushambuliaji raia na walinda amani kiholela, na mauaji na taabu inayosababishwa na mzozo huo kwa watu wa Sudan Kusini.

Katibu Mkuu amelaani vikali kulengwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali, majengo yao, na mali zao mjini Juba, kunakoidaiwa kufanywa na wanajeshi wa SPLA, pamoja na ripoti za ukatili wa kingono, uvamizi na mauaji ya wafanyakazi hao na raia wa Sudan Kusini wasio na hatia.

Katibu Mkuu ameuambia mkutano wa IGAD kuwa sasa ndio wakati wa kuchukua hatua madhubuti kwa pamoja, kwani watu wa Sudan Kusini wanahitaji kusikia kwamba ukanda na ulimwengu unanena kwa sauti moja ili kumaliza machafuko hayo yasiyo na maana nchini mwao.

Ban amesema sasa ndio wakati wa kutuma ujumbe mzito kwa viongozi wa Sudan Kusini, kwamba wamewafeli watu wao, na kwamba matumaini na ndoto zao zimevurugwa kwa sababu ya pande zinazozozana kutaka kujinufaisha na kujipatia mamlaka binafsi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter