Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu yaongezeka kwa kutoweka mamia ya wanaume na wavulana Fallujah:

Hofu yaongezeka kwa kutoweka mamia ya wanaume na wavulana Fallujah:

Nchini Iraq hofu inaongezeka kufuatia wanaume na wavulana zaidi ya 600 kuripotiwa kuchukuliwa mateka na wanamgambo wenye silaha baada ya kuangukia kwa waasi mji wa Fallujah mwezi uliopita, umesema Umoja wa Mataifa.

Katika wito wa kutafutwa na kuachiliwa watu hao, Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema tukio hilo linahatarisha kuzuka ghasia za kidini.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu, watu waliotoweka waliondoka kijijini kwao karibu na mji wa Fallujah mwezi Juni na walilazimika kusaka hifadhi na wapiganaji wa Kishia wanajisingizia kuwa wanjeshi wa serikali.

Mashahidi wanasema wanaume na vijana hao walitenganishwa na wanawake na watoto, na kuteswa vibaya. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(SAUTI YA COLVILLE)

“Mashahidi kadhaa wameeleza kwamba baadhi ya watu hao walioomba maji ya kunywa au kulalamika kuhusu kukosa hewa, waliburuzwa nje na kupigwa risasi, kunyongwa au kupigwa vibaya. Zaidi ya hayo mashahidi wamesema kwamba takribani watu wanne walikatwa vichwa. Wengine walitiwa pingu na kupigwa hadi kufa, na miili ya wanaume wawili ilitiwa moto."

Kamishina Zeid ametoa wito wa hatua za haraka kutoka kwa serikali ya Iraq kuwafikisha wahusika wa uhalifu huo mbele ya mkono wa sheria.