Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji wa kigeni wapungua kwa asilimia Saba Afrika-UNCTAD

Uwekezaji wa kigeni wapungua kwa asilimia Saba Afrika-UNCTAD

Ripoti mpya ya uwekezaji duniani imeonyesha kuwa mwaka jana uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, FDI duniani kwa ujumla uliongezeka na kufikia kiwango cha juu kabisa tangu mdororo wa kiuchumi.

Katika ripoti hiyo iliyotolewa leo na kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, uwekezaji wa kigeni kwa ujumla ulifikia dola zaidi ya trilioni Moja na nusu ikiwa ni ongezeko kwa asilimia 38.

Katibu Mkuu wa UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi amesema ongezeko hilo linatokana na ubia na ununuzi wa kampuni za mataifa mbali mbali ambapo nchi zinazoendelea barani Asia ndio zilikuwa kidedea kwa kupata uwekezaji mkubwa.

Hata hivyo hali si shwari kwa bara la Afrika ambapo uwekezaji wa kigeni ulipungua kwa asilimia Saba na kufikia dola bilioni 54.

Sababu kubwa la anguko limetajwa kuwa ni bei ya chini ya bidhaa iliyodidimiza uwekezaji wa kigeni katika nchi zenye uchumi unaotegemea maliasili.

UNCTAD inasema mwaka huu wa 2016 kuna matumaini ya kuongezeka kwa FDI kutokana na mipango ya kuwa na miradi isiyoharibu mazingira, kuweka biashara huru zaidi na kubinafsisha mashirika yanayomilikiwa na serikali.