Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatangaza mwisho wa dharura ya Ebola kimataifa

WHO yatangaza mwisho wa dharura ya Ebola kimataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza leo kuwa mlipuko wa maambukizi ya virusi vya homa ya Ebola siyo tena suala la dharura linalotishia afya ya umma kimataifa, na kwamba hatari ya kuenea maambukizi ya Ebola kimataifa ni ndogo sana, kwani nchi sasa zina uwezo wa kukabiliana haraka na milipuko mipya.

Tangazo hilo limefuatia mkutano wa tisa wa Kamati ya Dharura ya WHO, kuhusu mlipuko wa homa ya Ebola Afrika Magharibi, ambao umefanyika kwa njia ya simu leo Machi 29, 2016 kuanzia saa sita na nusu hadi saa tisa na nusu za Geneva.

Mkutano huo ulioitishwa na Mkurgenzi Mkuu wa WHO, Dr. Margaret Chan, uliombwa kutoa maoni na mwelekeo kuhusu iwapo mlipuko wa Ebola bado ni suala la dharura linalotishia afya ya umma kimataifa, na umejumuisha wawakilishi kutoka nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Wawakilishi hao wa nchi tatu zilizoathiriwa zaidi na mlipuko wa Ebola wamewasilisha ripoti zao kuhusu hali ya homa hiyo katika nchi zao, na kazi inayoendelea ya kuzuia kuzuka tena kwa maambukizi ya virusi vya Ebola, pamoja na uwezo wa kugundua na kukabiliana hima na visa vyovyote vipya vya virusi hivyo.