Skip to main content

Balozi Kamau wa Kenya amulika mchango wa wanawake katika masuala ya amani

Balozi Kamau wa Kenya amulika mchango wa wanawake katika masuala ya amani

Ushiriki wa wanawake katika utaratibu wa kujenga amani ni suala la msingi katika kudumisha amani, amesema leo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ujenzi wa amani kwenye Baraza la Usalama, Balozi Macharia Kamau, ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa.

Akihutubia kikao maalum cha Baraza hilo kilichofanyika leo kuhusu wanawake katika utaratibu wa kuzuia na kutatua mizozo barani Afrika, Balozi Kamau amesema licha ya kutengwa kwenye ngazi za uongozi na kutopewa nafasi za kutosha kwenye taratibu za ujenzi wa amani, wanawake wanachangia pakubwa kwenye ngazi za jamii katika kuzuia mizozo.

“Ingawa mikakati ya kitaifa ya Kamisheni ya Ujenzi wa Amani inatambua mchango wa wanawake katika kujenga amani, kuzigeuza ahadi rasmi kuwa hatua madhubuti katika mazingira halisi hakujawa na utaratibu na ufanisi upasao. Matarajio makubwa kuhusu mabadiliko makubwa na kuimarishwa kwa ushiriki wa wanawake katika amani na usalama yalivyotazamiwa katika azimio namba 1325 (la Baraza la Usalama), hayajatimizwa.”

Amesisitiza umuhimu wa kuwezesha hatua hizo za ngazi za jamii akisema Kamisheni anayosimamia hivi sasa inaandaa mkakati maalum kuhusu usawa wa jinsia kwenye ujenzi wa amani, unaotarajiwa kuwasilishwa mbele ya Baraza la Usalama mwezi Julai mwaka huu.

Aidha Balozi Kamau amemulika mifano iliyoleta mafanikio tayari, akitaja Burundi ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, limesaidia wanawake zaidi ya 500 vijijini nchini humo ambao kwa mujibu wa shirika hilo, wameza kukabiliana na mizozo zaidi ya 5,000 mwaka 2015 na hivyo kupunguza mivutano ya kisiasa.