Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano thabiti wahitajika kwa janga la wakimbizi- Grandi

Mshikamano thabiti wahitajika kwa janga la wakimbizi- Grandi

Hii leo ni miaka mitano tangu kuanza kwa mzozo wa Syria ambapo mapigano bado yanaendelea na raia wanaokimbia zahma hiyo wakikumbwa na vikwazo wanaposaka hifadhi kwingineko ikiwemo Ulaya. Amina Hassan na ripoti kamili.

(Taarifa ya Amina)

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi amesema Syria ni janga kubwa la kibinadamu na ukimbizi kwa zama za sasa likihitaji mshikamano zaidi siyo tu kusaka suluhu ya kisiasa bali pia kuwapatia hifadhi wakimbizi hao.

Amesema licha ya nuru katika usambazaji misaada hivi sasa, pamoja na kurejea kwa mazungumzo ya kusaka suluhu na ahadi za usaidizi wa kifedha, giza nene limetanda huko mipakani ambako wakimbizi wanakimbilia kuokoa maisha yao, udhibiti ukiwa ni mkali zaidi.

Bwana Grandi amesema hali hiyo inasababisha maelfu ya raia walio hatarini kukwama Syria, kwa kuwa nchi za Ulaya ambazo awali ziliwakaribisha sasa zimefunga milango kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi kusaka hifadhi kwenye nchi zao.

Wakati huo huo, balozi mwema wa UNHCR Angelina Jolie ametembelea kambi ya wakimbizi wa Syria huko bonde la Bekaa nchini Lebanon akipaza sauti mzozo wa Syria upatiwe suluhu haraka...

(Sauti  ya Jolie)

"Ombi langu leo ni kwamba tunahitaji serikali duniani kote kuonyesha uongozi : kuchambua hali na kuelewa nini hasa kila nchi inaweza kufanya,  wakimbizi wangapi inaweza kusaidia na jinsi gani, kuelezea hiyo kwa wananchi wao na kukabiliana na hofu."