Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adhabu kali kwa madawa ya kulevya hazitimizi haki- UNODC

Adhabu kali kwa madawa ya kulevya hazitimizi haki- UNODC

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC), Yury Fedotov, amesema kuwa njia mbadala zinaweza kutumiwa na serikali dhidi ya makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya, badala ya vifungo au adhabu, kulingana na mikataba ya kimataifa ya kudhibiti madawa.

Akizungumza wakati wa kikao cha 59 cha Kamisheni kuhusu Madawa ya Kulevya mjini Vienna, Bwana Fedotov amesema makabiliano makali kupindukia dhidi ya wanaotenda makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya hayasaidii kuendeleza haki wala utawala wa sheria.

Mkuu huyo wa UNODC amesema njia mbadala zitasaidia kushughulikia changamoto za msongamano magerezani na zinaweza pia kuzuia hatari ya wafungwa wengine kusajiliwa na wahalifu na magaidi katika vikundi vyao.

Akitoa mfano, amesema adhabu ya kifo haijawahi kuwekwa katika mikataba ya kimataifa kuhusu madawa, kwani adhabu kali hazitimizi haki au kuendeleza utawala wa sheria.