Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya ukatili wa kingono kutoka kwa walinda amani UM viliongezeka- Ripoti

Visa vya ukatili wa kingono kutoka kwa walinda amani UM viliongezeka- Ripoti

Idadi ya visa vya ukatili na unyanyasaji wa kingono vinavyodaiwa kutekelezwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2015 vimeongezeka hadi 69 ikiwa ni ongezeko kutoka visa 52 mwaka uliotangulia.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon iliyowasilishwa na msaidizi wake wa masuala ya operesheni mashinani Atul Khare mbele ya waandishi wa habari jijini New York, Marekani leo.

Bwana Khare amesema visa viliongezeka zaidi kutokana na matukio 22 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR yaliyotekelezwa na walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA.

Hata hivyo amesema Katibu Mkuu katika ripoti yake ametangaza hatua ambazo pamoja na mambo mengine zinalenga kulinda wahanga, kuhakikisha watendaji hawakwepi sheria halikadhalika kuzuia visa hivyo.

Mathalani amesema kwa kuhakikisha watendaji hawakwepi sheria..

(Sauti ya Khare-1)

“Katibu Mkuu ameziomba nchi wanachama kuunda mahakama za kijeshi kule kwenye vikosi vyao pindi kunaibuka madai ya visa vya  ukatili wa kingono, halikadhalika kuweka sheria za nchi zao kuhusu suala hilo. Wakati nchi zinafikiria ombi hilo, napenda kupongeza kwa dhati Afrika Kusini ambayo iliamua kuendesha mahakama ya kijeshi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”

image
Walinda amani wa MONUSCO wakiwa kwenye doria huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. (Picha:UN /Sylvain Liecht)
Na kwa upande kwa wahanga wa visa vya ukatili wa kingono, iwapo kuna ujauzito..

(Sauti ya Khare-2)

“Katibu mkuu ameomba nchi wanachama kupokea malalamiko kutoka kwa wahanga kuhusu usaidizi wa kifedha. Halikadhalika ameomba nchi zote zinazochangia polisi na askari kuteua kitengo kitakachofuatilia madai yanayohusu kusaka baba wa watoto.”

image
Mkuu wa MINUSCA Parfait Onanga-Anyanga (katikati na shati jeupe) akizungumza na wananchi. (Picha/MINUSCA-Flickr)
Kuhusu adhabu zinazotolewa na nchi husika kwa wale wanaobainika kutenda makosa, Bwana Khare ametoa ombi..

(Sauti ya Khare-3)

“Lakini pia tunatoa wito kwa nchi wanachama kuhakikisha adhabu inayotolewa inaendana sambamba na ukubwa wa kosa na hatimaye taratibu za jinai zinafuata. Katika matukio mengine tumeshuhudia adhabu ambazo hazilingani na kosa husika hivyo tumeomba nchi husika kuchukua hatua mujarabu ikiwemo kukata rufaa kwenye mahakama za nchi zao.”

Amerejelea wito wa Ban wa kutaka nchi kuchukua hatua za kinga zaidi dhidi ya matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kingono huku akisema wataanzisha mafunzo kupitia mtandao kama njia mojawapo ya kuzuia vitendo hivyo vinavyofanywa na walinda amani.