Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon aeleza dhamira yake kuchangia amani Sahara Magharibi

Ban Ki-moon aeleza dhamira yake kuchangia amani Sahara Magharibi

Akiwa ziarani Mauritania kwa ajili ya kufuatilia hali ya Sahara Magharibi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kwamba anataka kuchangia katika kutafuta suluhu kwa mzozo uliodumu kwa muda mrefu.

Aidha amezungumzia ukosefu wa usalama kwenye ukanda wa Sahel, akisisitizia umuhimu wa kukabiliana na mizizi yake, ikiwa ni umaskini, ukosefu wa ajira, ubaguzi na ukiukaji wa haki.

Katibu Mkuu ameipongeza Mauritania kwa mafanikio yake katika kukuza demokrasia na ujumuishi wa kijamii, akiisihi serikali kuendelea kutunza haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, na kupambana na utumwa unaoendelea kufanyika nchini humo.

Baada ya ziara yake Mauritania, bwana Ban anatarajia kutembelea Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwenye Sahara Magharibi, na kukutana na wakimbizi kutoka eneo hilo.

Wakati huo huo Ban amehudhuria mkutano kuhusu amani an usalama ukanda wa Sahel na jinsi ya kushughulikia vyanzo vya ukosefu wa utulivu kwenye ukanda huo, uliofanyika kwenye mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott. Amesema ukanda wa Sahel barani Afrika unakabiliwa na hatari kuu tatu akizitaja kuwa ni uharibifu wa mazingira, umaskini na ukosefu wa usalama.