Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wataka haki za wanawake vijijini ziheshimiwe

Wataalam wa UM wataka haki za wanawake vijijini ziheshimiwe

Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, wataalam wa Umoja wa Mataifa wametoa wito haki za wanawake wa vijijini ziheshimiwe, na mchango wao katika maendeleo na kupunguza umaskini utambuliwe. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Wataalam hao wa Kamati ya Kutokomeza Ubaguzi Dhidi ya Wanawake, (CEDAW), wametaka wamulikwe wanawake na wasichana wa vijijini, na kutekeleza ipasavyo malengo ya maendeleo endelevu, (SDGs), ambayo kwa wingi yanalenga hali ya wanawake vijijini.

Wamesisitiza haja ya kulinda na kuendeleza haki za wanawake na wasichana vijijini, wakisema kuwa wanawake hao ambao ni robo ya idadi ya watu duniani, hukumbana na changamoto za kimfumo na vizuizi katika kufurahia haki zao kikamilifu.

Wameongeza kuwa katika nchi nyingi, mahitaji ya aina yake ya wanawake hao hayashughulikiwi katika sheria, katika sera za kitaifa na mikoa, na katika bajeti.