Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vizuizi vya mipakani huathiri zaidi watoto wakimbizi na wahamiaji- UNICEF

Vizuizi vya mipakani huathiri zaidi watoto wakimbizi na wahamiaji- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema kuwa hali mbaya inayoibuka kwenye mipaka ya nchi za mashariki mwa Ulaya, hususan Ugiriki na Jamhuri ya zamani ya Yugoslavia ya Macedonia, imewaacha maelfu ya watoto wakihaha kwa taabu na hatari ya kuathiriwa kiafya na kunyanyaswa.

UNICEF imesema, katika mazingira hayo magumu, watoto wamelazimika kulala nje, mara nyingi kwa zaidi ya wiki moja, wakikosa huduma za msingi kama maji na chakula.

Aidha, familia zinawekwa katika hatari ya kutenganishwa, watoto wakikwama katika vituo vya muda kwa kipindi kirefu, bila kujua hatma yao au wanakokwenda.

Shirika la UNICEF limekuwa likitoa huduma za maji, kujisafi na chakula kwa watoto na familia zao, ili angaa waweze kujikimu katika mazingira hayo magumu.