Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu yatafuta mbinu mbadala nchini DRC

Mashirika ya kibinadamu yatafuta mbinu mbadala nchini DRC

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Condo DRC Dokta Mamadou Diallo amesema dola milioni 690 zinahitajika ili kukabiliana na athari za mzozo huo uliodumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Daktari Diallo ameeleza kwamba mashirika ya kibinadamu yanajaribu kuwezesha zaidi serikali za mitaa katika kuhudumia wananchi milioni 6 wanaohitaji msaada nchini humo.

Amesema wanajaribu pia kubuni vyanzo vipya vya ufadhili ikiwemo kwa kushirikisha kampuni za binafsi na wawekezaji wanaonufaika na rasilimali za DRC.

Kadhalika amemulika umuhimu wa kutafuta suluhu endelevu kwa mzozo wa kibinadamu.

(Sauti ya Dkt Diallo)

"Suluhu ya muda mrefu nchini DRC siyo kuendelea kukabiliana na mahitaji yanayoibuka, bali ni kujaribu kuyapunguza kadri inavyowezekana. Inamaanisha kubuni suluhu mbadala kukabiliana na sababu za msingi za mzozo huo, ambazo hasa zinahusiana na siasa na ukosefu wa usalama kwa muda mrefu kwenye baadhi ya maeneo ya nchi hii."