Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AU yazindua siku ya mlo shuleni, umuhimu wake wawekwa bayana

AU yazindua siku ya mlo shuleni, umuhimu wake wawekwa bayana

Kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP zimekaribisha uzinduzi wa siku ya mlo shuleni barani Afrika hii leo ikiwa ni ishara ya AU kutambua umuhimu wa mlo katika makazi na kuboresha elimu.

Uzinduzi umefanyika Roma, Italia ambapo taasisi hizo mbili zimesema mlo shuleni huchochea watoto kwenda shule na kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula katika eneo husika kwa kuwa chakula kinacholimwa ndio kinapatiwa pia watoto.

Mkurugenzi Mkuu wa WFP Etharin Cousin amesema sambamba na hilo mlo shuleni husaidia kukuza uchumi wa eneo husika kwani watoto wanapokwenda shule wanasaidia kuboresha mustakhbali wa eneo lao.

Naye Mkuu wa kamisheni ya AU Nkosazana Dlamini-Zuma amesema mpango wa mlo shule umenufaisha wengi akiwemo yeye mwenyewe na kuwawezesha kufika walipo leo hii.

Mwaka 2014, mpango wa mlo shuleni unaopigiwa chepuo na WFP ulinufaisha watoto zaidi ya Milioni 10 katika nchi 41 barani Afrika.

Ulimwenguni zaidi ya watoto Milioni 370 katika nchi 131 wananufaika na mipango ya mlo shuleni inayosimamiwa na serikali.