Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjini Goma, Ban akutana na mkombozi wa wanawake, Daktari Mukwege

Mjini Goma, Ban akutana na mkombozi wa wanawake, Daktari Mukwege

Akiwa ziarani mashariki mwa DRC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana na Daktari Denis Mukwege, ambaye ni mkuu wa hospitali ya Panzi Kivu Kusini inayoshughulikia kutibu na kupasua wanawake walioathirika na ubakaji nchini humo.

Akizungumza na Bernardin Nyangi wa Redio ya Umoja wa Mataifa, Radio OKAPI baada ya mazungumzo ya ana kwa ana na Katibu Mkuu, Daktari Mukwege amesema mafanikio makubwa yalipatikana katika juhudi za kupambana na ubakaji kwenye maeneo ya Kivu, kwa ushirikiano na wadau mbali mbali na Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo akaongeza kwamba hatua zaidi za kisheria zinahitajika.

(Sauti ya Daktari Mukwege)

"Tumezungumza zaidi kuhusu mafanikio yaliyopatikana. Kwa kweli, wanawake walionufaika na huduma zetu wanachotarajia sasa baada ya mkutano huo ni juhudi zaidi. Hadi sasa tunasikitishwa na kwamba, hata wakati ambapo wanawake wanashinda kesi zao, bado hakuna malipo yoyote yanayotolewa. Ni muhimu wanawake hawa warudishiwe haki ili kuwasaidia kupona kabisa, na jamii iwakubali kwamba ni wahanga wa ubakaji badala ya kuwabagua."