Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutambuliwe kama wanasayansi siyo wanawake kwenye sayansi: Nisreen

Tutambuliwe kama wanasayansi siyo wanawake kwenye sayansi: Nisreen

Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake na watoto wa kike katika fani ya sayansi, ikiwa ni mara ya kwanza siku hii kuadhimishwa baada ya Umoja wa Mataifa kupitisha azimio mwezi Disemba mwaka jana kwa lengo la kushawishi kundi hilo kujiunga katika fani hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano huo Nisreen el-Hashemite ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kimataifa ya kifalme kuhusu sayansi amesema ni wakati wa kubadili mtazamo kwa wanawake walioko kwenye fani hiyo kwani mtazamo wa sasa unakwamisha ushiriki wao kwenye fani hiyo yenye nafasi kubwa kuleta maendeleo endelevu..

(Sauti ya Nisreen)

“Kwa mtazamo wangu malengo ya maendeleo endelevu kwa kiasi kikubwa yanahitaji msingi mkubwa wa sayansi na hii haiwezi kufanikiwa popote pale iwapo wanawake na watoto wa kike kushiriki kwenye fani hii. Kuanzia leo nina matumaini makubwa kuwa iko siku nitaitwa mwanasayansi badala ya mwanamke kwenye fani ya sayansi, na pia kutambuliwa kwa mafanikio yangu badala ya jinsia yangu.”

Bi. Nisreen ambaye yeye mwenyewe ni mwanasayansi ametaka mazingira bora kwa makundi hayo kwenye sayansi huku washiriki wengine wakitaka watunga sera kubadili mitazamo yao ikiwemo kuweka sera zinazochochea na kutoa fursa zaidi kwa wanawake na wasichana kwenye masomo ya sayansi.