Skip to main content

UM watangaza jopo la ngazi ya juu la uwezeshaji wanawake kiuchumi

UM watangaza jopo la ngazi ya juu la uwezeshaji wanawake kiuchumi

Mkutano wa jukwaa la uchumi ukiendelea huko Davos, Uswisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ametumia fursa hiyo kushiriki katika matukio mbali mbali ikiwemo kutangaza jopo la uwezeshaji wanawake kiuchumi duniani na kuzindua jopo la kusongesha malengo ya maendeleo endelevu. Flora Nducha na taarifa kamili.

(Taarifa ya Flora)

Jopo hilo la uwezeshaji wanawake ni la kwanza kabisa na lengo ni kutoa uongozi imara na kuandaa hatua madhubuti zenye lengo la kuziba pengo la kijinsia la kiuchumi ambalo limetawala duniani.

Jopo hilo litatoa mapendekezo kwa ajili ya utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu kwa ajili ya kuboresha matokeo ya kiuchumi kwa wanwake na kuchagiza uongozi kwa wanawake ili kusukuma mbele ajenda jumuishi, endelevu inayojali mazingira katika kukuza uchumi.

Ban amesema mapendekezo hayo muhimu ni kwa ajili ya hatua muhimu zitakazochukuliwa na serikali, sekta binafsi, mfumo wa Umoja wa Mataifa, na wadau wengine pamoja na sera zinazohitajika ili kufikia malengo mapya ya maendeleo endelevu ambayo yanatoa wito wa uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake.

Wakati huo huo Ban amezindua jopo alilotangaza hivi karibuni la kueneza na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au ajenda 2030 akisema kuyafahamu malengo tu haitoshi umuhimu ni....

(Sauti ya Ban)

“Utetezi, utetezi, hata kama una maono mazuri na bora ya namna gani! Kama unayahifadhi kwenye mfuko wako haisaidii na hamna atakayefahamu. Ndio maana tuko hapa! Lengo ni utetezi! Wafahamishe watu una dira gani na maono gani na yanajumuisha nini.”