Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na hatua tano za kuchukua hatua kuhimili mabadiliko ya tabianchi

Ban na hatua tano za kuchukua hatua kuhimili mabadiliko ya tabianchi

Mkutano wa jukwaa la uchumi duniani huko Davos, Uswisi ukiwa umeingia siku ya pili, mada kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na hatua za kuchukua imeangaziwa hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisema mwelekeo uko dhahiri.

Ban akizungumza kwenye moja ya mijadala amesema athari ziko dhahiri shahiri na zimejidhihirisha kila kona ya dunia ikiwa pia kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwaka 2012 yalipokumbwa na kimbunga Sandy.

Hivyo ametaja mambo makuu matano ya kuzingatia wakati huu ambapo dunia tayari imepitisha mkataba wa kudhibiti na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

(Sauti ya Ban)

“Mosi, mipango ya kitaifa kuhusu tabianchi lazima kwa haraka ibadilishwe na kuwa mikakati na miradi bora ya kutegemewa. Pili lazima tuchangishe fedha za kutosha ili kuachana na nishati kisukuku na kukidhi mahitaji ya nishati isiyo na hewa ya ukaa. Tatu tunahitaji rasilimali na umakini katika mbinu za kuhimili tabianchi. Nne tunapaswa kuongeza haraka hatua kuhusu tabianchi na tano serikali lazima ziridhie haraka mkataba wa Paris ili uanze kutumika.”

Ban amesema anatambua kuwa matrilioni ya dola yatawekezwa katika miundombinu siku za usoni lakin ni vyema kukumbuka kuwa miundo iliyozoeleka ya maendeleo inachochea mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo amesema ni vyema kuchukua hatua  na hivyo sekta binafsi ina fursa kubwa kuchagiza na kueneza nishati salama.