Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji muhimu yafikia walionasa kwenye mapigano Madaya, Syria

Mahitaji muhimu yafikia walionasa kwenye mapigano Madaya, Syria

Hatimaye msafara wa magari yaliyobeba shehena za bidhaa muhimu za kuokoa uhai wa binadamu walio kwenye maeneo yaliyoshikiliwa huko Syria, umewasili kwenye mji wa Madaya nchini humo.

Shehena ni pamoja na vifaa tiba, vyakula na mablanketi kutoka Umoja wa Mataifa na washirika wake na lengo ni kufikia wakazi 42,000 ambao wameripotiwa kukumbwa na njaa kutokana na eneo lao kuzingirwa na vikosi vinavyounga mkono serikali.

Wakati huo huo, imeripotiwa kuwa malori yameondoka mji mkuu Damascus kuelekea maeneo ya Kafraya na Foah, miji ambayo inashikiliwa na vikosi vya upinzani nchini Syria kwa mwaka wa sita sasa.

Shirika lisilo la kiserikali la madaktari wasio na mipaka, MSF limesema mwezi Disemba mwaka jana watu 23 walifariki dunia kutokana na njaa kwenye miji hiyo na kwamba Sita kati yao walikuwa ni watoto.

Kwa mujibu wa MSF, watu wanaotaka kukimbia miji hiyo wameripotiwa kuuuawa.