Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Karen AbuZayd ndiye mshauri wa mkutano wa masuala ya wakimbizi na wahamiaji

Karen AbuZayd ndiye mshauri wa mkutano wa masuala ya wakimbizi na wahamiaji

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ametangaza leo uteuzi wa Bi Karen AbuZayd wa Marekani kama mshauri maalumu wa mkutano wa kushughulikia wimbi kubwa la uhamaji wa wakimbizi na wahamiaji ambao utafanyika kwenye baraza kuu la umoja wa Mataifa mwezi septemba 2016.

Mshauri huyo maalumu atafanya kazi kwa karibu na vyombo vya Umoja wa Mataifa na kufanya mashauriano nan chi wanachama na wadau wengine hadi wakati wa mkutano huo.

Hii ni pamoja na kusimamia ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu harakati kubwa za wakimbizi na wahamiaji itakayowasilishwa kwenye baraza kuu mwezi Mai mwaka huu. Bi AbuZayd ana ujuzi mkubwa kuhusu masuala ya misaada na haki za binadamu baada ya kufanya kazi katika nchi mbalimbali.

Tangu mwaka 2011 amekuwa akifanya kazi kama kamishina wa tume huru ya uchunguzi kuhusu Syria, mwaka 2005 aliteuliwa kuwa kamishina mkuu wa UNRWA shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina , kazi aliyohudumu kwa miaka mitano.

Lakini kabla ya hapo kwa miaka 19 amefanya kazi na ofisi ya kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. Pia aliwahi kuwa mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa Bosnia na mhadhiri katika chuo kikuu cha Makerere Kampala Uganda.