Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wang’oa zaidi ya watoto Milioni Moja shuleni Nigeria

Mgogoro wang’oa zaidi ya watoto Milioni Moja shuleni Nigeria

Mgogoro unaoendelea kaskazini-mashariki mwa Nigeria na nchi  jirani umesababisha zaidi ya watoto  Milioni Moja kuacha shule.

Hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF likisema idadi hiyo inaongeza idadi ya watoto Milioni 11 nchini Nigeria, Cameroon, Chad na Niger wenye umri wa kwenda shule lakini wamekuwa hawaendi tangu kuibuka kwa mzozo huo.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Afrika Magharibi, Manuel Fontaine amesema ni idadi ya kutisha na ni pigo kubwa kwa sekta ya elimu katika ukanda huo kwani licha ya kusababisha watoto kushindwa kwenda shule, inaweza kusababisha waache kabisa fursa ya elimu.

Nchini Nigeria, Cameroon, Chad na Niger, zaidi ya shule 2,000 hazijafunguliwa kutokana na mzozo unaotokana na mashambulizi ya Boko Haram.

UNICEF na wadau inatekeleza mpango wa kusaidia watoto kurejea shuleni ambapo hadi sasa imesaidia watoto 170,000 kwenye maeneo salama.

Hata hivyo Fontaine amesema changamoto ni kuhakikisha watoto hao wako salama na hawakatizi masomo yao.

Kwa mujibu wa UNICEF, mwaka 2016, itahitaji dola Milioni 23 ili kuwezesha watoto kupata elimu katika mataifa hayo manne hususan wale wanaoishi kando mwa ziwa Chad.