Misaada ya kibinadamu kufikishwa Taizz Yemen

17 Disemba 2015

Mazungumzo ya amani ya Yemen yakiendelea nchini Uswisi, washiriki wameafikiana kuhusu kurejesha mara moja usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwenye mji wa Taizz nchini humo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed amekaribisha muafaka huo akisema ni hatua muhimu katika kupunguza mateso ya raia wa Yemen.

Tayari msafara wa Umoja wa Mataifa uliobeba vifaa vya msingi vya kibinadamu umefika Taizz na kwenye siku chache zijazo misaada hiyo itaanza kusambazwa maeneo yaliyoathirika zaidi.

Bwana Ahmed amepongeza washiriki wa mazungumzo hayo kwa mafanikio hayo akiwasihi kuendeleza bidii ili kuafikiana kuhusu hatua zingine zitakazowezesha usaidizi wa kibinadamu kufikia raia wa Yemen nchini kote.

Mazungumzo ya amani yanatarajia kuendelea ili kuafikia kuhusu sitisho la mapigano, kuachiliwa kwa wafungwa, kusalimisha kwa silaha na kurejesha utawala wa sheria na mazungumzo ya kisiasa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter