Skip to main content

Pakaza rangi ya chungwa! Kampeni dhidi ya ukatili kwa wanawake

Pakaza rangi ya chungwa! Kampeni dhidi ya ukatili kwa wanawake

Uzinduzi rasmi wa siku 16 za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike unafanyika maeneo mbali mbali dunia kesho tarehe 25 Novemba , sambamba na siku ya kimataifa ya kutokomeza vitendo hivyo ambapo kunatarajiwa kuwepo kwa matukio zaidi ya 450 ikiwemo maandamano, mijadala mashuleni na hata mechi za soka, ujumbe mkuu ukiwa pakaza rangi ya chungwa ulimwenguni.

Taarifa iliyotolewa Jumanne na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women kampeni hiyo inalenga kuchagiza kumalizika kwa vitendo hivyo kama vile ukeketaji, ubakaji ndani ya ndoa na ukatili majumbani vinayokumba mwanamke mmoja kati ya kila watatu duniani kote.

Kampeni ya mwaka huu inajikita zaidi katika ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endelevu ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema ukatili dhidi ya wanawake na watoto unasalia kuwa moja ya ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu unaovumiliwa.

Amesema ukatili huo ni matokeo ya ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi na kwamba ni kiashiria cha jamii ambayo inakosa mizania na hivyo ni lazima kuutokomeza.

Hata hivyo Bi Mlambo-Ngucka amepongeza nchi ambazo zimechukua hatua akisema hadi leo nchi 125 zimepitisha sheria za kudhibiti ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto wa kike, nchi 119 zina sheria dhidi ya ukatili majumbani lakini ni nchi 52 tu zenye sheria dhidi ya ubakaji ndani ya ndoa.

Kwa mantiki hiyo amesema ajenda 2030 ni fursa ya kuchochea uwepo wa dunia inayojali ustawi wa makundi yote bila kujali jinsia zao.