Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuta na madini vyaweza ongeza ajira Afrika:UNCTAD

Mafuta na madini vyaweza ongeza ajira Afrika:UNCTAD

Huko Khartoum nchini Sudan kunafanyika mkutano kuhusu machimbo ya mafuta sambamba na maonyesho kuhusu sekta hiyo, kinachoangaziwa zaidi ikiwa ni jinsi sekta hiyo inaweza kuzalisha ajira zaidi kwenye uchumi.

Taarifa iliyotolewa leo na kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD inasema sekta ya mafuta na gesi kwa sasa inaajiri asilimia Moja tu ya wafanyakazi barani Afrika wakati kila mwaka vijana Milioni 12 wanaingia soko la ajira, kati yao Milioni tano tu wakiajiriwa. .

Utafiti wa UNCTAD umeonyesha kwamba ajira moja kwenye sekta ya madini nchini Ghana inaweza kuzalisha ajira hadi 27 kwenye uchumi mzima.

Kwa mujibu wa UNCTAD bara la Afrika lina asilimia Nane ya akiba yote za mafuta na gesi duniani huku likiwa la kwanza kwa akiba ya madini mbalimbali kama vile boksiti, kobalti, almasi na manganizi.