Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Weledi kwa polisi walinda amani ni muhimu sasa kuliko wakati wowote: Ladsous

Weledi kwa polisi walinda amani ni muhimu sasa kuliko wakati wowote: Ladsous

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala kuhusu dhima ya polisi kwenye shughuli zake za ulinzi wa amani hususan kwenye operesheni ambazo zinakuwa na jukumu la ulinzi wa raia. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Mjadala huo umefanyika ikiwa ni hitimisho la wiki ya Polisi ndani ya Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia kupanuka kwa wigo wa shughuli za polisi kwenye operesheni za ulinzi wa amani.

Makamishna wakuu wa polisi kwenye operesheni hizo wameshiriki ambapo Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amesema weledi ni jambo la msingi kwa polisi wanaoshiriki katika ulinzi wa raia.

(Sauti ya Ladsous)

Tunahitaji kufanya kila kitu kuendelea kutoa mafunzo ya weledi kwa vikosi vyetu vya polisi  ili viweze kukabiliana na changamoto (faire face) na kutumia ipasavyo vikosi vya polisi vilivyo tayari kwa ajili ya operesheni. Nadhani ni muhimu sana."

Na mwisho ni ombi kwa Baraza la usalama..

(Sauti ya Ladsous)

Ningependa kutoa ombi kwa baraza la usalama liendelee kuwa wazi kwa kadri inavyowezekana kila wakati linapotupatia ombi na ushauri. Tunaweza kufanya kazi kwa uthabiti iwapo tuna mkakati wa wazi wa kisiasa na iwapo tunaungwa mkono nanyie kuhusiana na nchi mwenyeji ambazo mara nyingine hazina uelewa tungeoupenda."  

Bwana Ladsous amesisitiza licha ya polisi wa Umoja wa Mataifa unashiriki katika ulinzi wa raia bado nchi husika ndiyo yenye jukumu kubwa la kulinda raia wake.