Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi duniani watakiwa kuweka lengo endelevu wakati wa COP21

Viongozi duniani watakiwa kuweka lengo endelevu wakati wa COP21

Viongozi wa kampuni na asasi za kiraia 22 kutoka sehemu mbalimbali, wamewaandikia barua wakuu wa nchi kote duniani wakiwataka kuwajibika katika kuhakikisha kuwa lengo nyoofu na la muda mrefu ni sehemu ya makubaliano katika mkutano ujao wa mabadilio ya tabianchi, COP21. Assumpta Massoi na maelezo kamili.

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Ikiwa ni yamesalia takribani majuma mawili kuelekea COP21 mjini Paris Ufaransa, huku viongozi wa nchi zenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani G20 wakikutana juma hili, barua hiyo imesema ni wakati muhimu kwa viongozi kusikia kwamba biashara inasaidia makubaliano kabambe yatakayofikiwa mjini Paris.

Barua hiyo imefafanua kuwa lengo la muda mrefu ni muhimu kwani litahamasisha uchumi na rasilimali watu na kuvutia sekta binafsi kuwekeza ili kufanikisha uchumi rafiki kwa mazingira.

Halikadhalika barua hiyo ya makampuni na asasi hizo 22 ikiwemo Safaricom yas Kenya imesisitiza kukomesha uzalishaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050 .