Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waandishi 700 wauawa kwa kipindi cha miaka 10, Umoja wa Mataifa wataka hatua

Waandishi 700 wauawa kwa kipindi cha miaka 10, Umoja wa Mataifa wataka hatua

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji sheria kwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemulika umuhimu wa kutunza haki zao huku waandishi 700 wakiwa wameuawa kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kwenye ujumbe wake kwa siku hiyo, Bwana Ban amesema ni asilimia Saba tu ya kesi za uhalifu dhidi ya waandishi wa habari ambazo zinafuatiliwa kisheria, akiongeza kwamba hilo linaongeza hofu miongoni mwa waandishi huku serikali zikiwadhibiti.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni, Sayansi na Elimu UNESCO Irina Bokova amesema ni lazima kuongeza bidii ili kutokomeza ukwepaji sheria wakati ambapo mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari yanazidi kuongezeka.

Bi Bokova amesema UNESCO imeunda mpango kazi wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo, ambao tayari umeanza kupata mafanikio huku baadhi ya serikali zikiwa zimechukua hatua za kuimarisha usalama wa waandishi wa habari.