Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upinzani Cambodia mashakani: Ofisi ya Haki za Binadamu

Upinzani Cambodia mashakani: Ofisi ya Haki za Binadamu

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza wasiwasi wake kuhusu Cambodia ambapo imesema hali inazidi kuwa mbaya kwa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu.

Msemaji wa ofisi hiyo Ravina Shamdasani amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Uswisi, akisema kwamba wanasiasa 11 wamefungwa gerezani wakiwa wamepewa adhabu za vifungo vya kati ya miaka 7 hadi 20.

Aidha ameeleza kwamba jumatatu wiki hii kundi la wafuasi wa serikali lilishambulia na kuwapiga wabunge wa upinzani huku polisi ikiripotiwa kuangalia bila kuzuia kitendo hicho.

Akikaribisha kuanzishwa kwa tume ya uchunguzi kuhusu shambulio la jumatatu, Bi Shamdasani amesema :

¨Tunasisitiza kwamba haki ya kuandamana kwa amani na kujieleza huru ni haki ya kila mtu bila kujali maoni yake ya kisiasa. Tunasihi pia serikali ichukue hatua zote zinazohitajika ili kuhakikishia usalama wa wabunge wote waliohaguliwa kwa njia ya demokrasia na raia wa Cambodia.¨