Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na usaidizi kwa wahanga wa shambulio dhidi ya wageni Grahamstown

UNHCR na usaidizi kwa wahanga wa shambulio dhidi ya wageni Grahamstown

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linashirikiana na mamlaka nchini Afrika Kusini kusaidia watu waliopoteza makazi yao kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya wageni kwenye kitongoji cha Grahamstown, jimbo la Eastern Cape.

Msemaji wa UNHCR kanda ya kusini mwa Afrika Tina Ghelli ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi hayo yalichochewa na madai ya raia wa kigeni kuhusika na mauaji ya mwenyeji, ambapo makazi ya watu yalichomwa moto na hata bidhaa kuporwa.

Bi. Ghelli amesema kile ambacho UNHCR inafanya hivi sasa.

(Sauti ya Ghelli)

“Tutaisaidia serikali na hatua zozote itakazochukua kama tulivyofanywa wakati wa matukio kama hayo kule Johannesburg na Durban. Kwa kuzingatia ripoti baada ya tathmini ya mahitaji, tutawapatia baadhi ya misaada ya misingi kwa watu waliopoteza makazi, labda kuwapatia makazi, vyakula na vifaa vya majumbani. Na pengine baadaye kuona jinsi ya kuwasaida wajenge upya maisha yao baada ya kupoteza mali zao kwenye mashambulizi.”