Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sababu saba zabainiwa kueleza wimbi la wakimbizi Ulaya

Sababu saba zabainiwa kueleza wimbi la wakimbizi Ulaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limebaini sababu saba zinazoeleza ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaotafuta hifadhi barani Ulaya baada ya kukimbia machafuko nchini  Syria.

Akiongea na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Mkurugenzi wa UNCHR kwa ukanda wa Mashariki ya Kati Amin Awad amesema watu milioni minne wamekimbia Syria na kusaka hifadhi nchi jirani za Jordan, Lebanon, Misri na Iraq tangu mwanzo wa mzozo na miongoni mwao zaidi ya 400,000 wameomba hifadhi barani Ulaya tangu mwaka 2011.

Kwa mujibu wake sababu ya kwanza ni kukata tamaa kuhusu hatma ya Syria, pili kukumbwa na umaskini kwenye nchi hizo jirani.

Aidha amesema wakimbizi wengi wameshindwa kupata kazi au ajira halali, wengi wakitumikiswa kwenye mazingira magumu .

Sababu nyingine iliyoelezwa na wakimbizi walioshiriki kwenye tathmini hiyo ya UNHCR ni kupunguka kwa misaada ya kimataifa, kukumbwa na matatizo mbalimbali wakati wa kuomba vitambulisho vya ukimbizi na kukosa fursa za elimu kwa watoto wao.

Hatimaye UNCHR imesema ukosefu wa usalama, hasa nchini Iraq, umesababisha watu wengi kutafuta hifadhi barani Ulaya.

Bwana Awad amesema cha msingi ni kuendelea kusaidia nchi hizo jirani

“ Nadhani suluhu ni kusaidia nchi kwenye ukanda huo, ili kuhakikisha utulivu nchini mwao, na kusaidia wakimbizi kwa kufadhili wito wa mashirika ya Umoja wa Mataifa,WFP, UNCHR, UNDP, WHO na  wadau wote wengi wa kimataifa na kitaifa ili waendelee kufanya kazi na kuleta utulivu. Pia, ni kuendelea kutafuta suluhu ya kisiasa kwa Syria.”