Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 34 wamefariki dunia kwa utapiamlo Bentiu- OCHA

Watoto 34 wamefariki dunia kwa utapiamlo Bentiu- OCHA

Shirika la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA, limesema leo kuwa watoto 34 walifariki dunia kutokana na utapiamlo katika kituo cha ulinzi wa raia, mjini Bentiu, jimbo la Unity, Sudan Kusini, katika wiki ya kwanza ya mwezi Septemba.

Katika taarifa yake, OCHA imesema idadi hiyo inazidi kiwango wastani cha dharura, ambacho ni vifo vya watu wawili katika kila 10,000 kwa siku, kwani kituo hicho cha Bentiu kinawapa hifadhi takriban wakimbizi wa ndani 112,000.

OCHA imeongeza kuwa sababu kuu ya vifo vya watoto ni malaria, huku sababu nyingine kuu zikiwa ni utapiamlo, surua, numonia na vidonda vilivyoambukizwa.

Utapiamlo linabakia kuwa tishio kubwa kote nchini Sudan Kusini, ambako takriban watoto robo milioni wana utapiamlo ulokithiri.