Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao wa Intaneti wa kasi ya juu bado haupatikani kwa watu bilioni 4 duniani

Mtandao wa Intaneti wa kasi ya juu bado haupatikani kwa watu bilioni 4 duniani

Bado asilimia 57 ya watu duniani kote hawawezi kutumia Intaneti kupitia mtandao wenye kasi ya juu zaidi yaani broadband.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Kamisheni ya Broadband kwa ajili ya maendeleo endelevu iliyotolewa leo, ikisema kwamba waliokosa mtandao huu ni watu wanaoishi kwenye nchi zinazoendelea na ambao wangenufaika zaidi na mtandao huo katika kujiendeleza kiuchumi na kijamii.

Ripoti imeonyesha kwamba asilimia 90 ya watu wanaoishi kwenye nchi 48 zilizokuwa maskini zaidi duniani hawapati kabisa mtandao wowote wa Intaneti, ikiwemo Burundi ambapo ni asilimia Moja Nukta Nne ya watu wanaoweza kutumia mtandao wa Intaneti.

Wakati ambapo viongozi wa kimataifa watakutana mwisho wa wiki hii kwa ajili ya kuridhia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, ripoti inasisitiza umuhimu wa teknolojia za habari na mawasiliano katika kutimiza malengo hayo yote na hasa yale yanayohusu huduma za afya, elimu na mazingira.

Kamisheni ya Broadband hushiriki wataalam na viongozi 50 kutoka sekta binafsi, serikali, Umoja wa Mataifa na asasi zisizo za kiserikali.