Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jeshi Burkina Faso lisiyumbishe mchakato wa kisiasa: IPU

Jeshi Burkina Faso lisiyumbishe mchakato wa kisiasa: IPU

Umoja wa mabunge duniani, IPU umelaani mapinduzi ya serikali ya mpito nchini Burkina Faso sanjari na kupelekwa mrama kwa mchakato wa kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini humo.

Katika taarifa yake Katibu Mkuu wa IPU Martin Chungong ametaka kurejeshwa haraka na kwa amani mchakato wa kidemokrasia utakaohitimishwa na uchaguzi huru na haki wa rais na wabunge mwezi ujao.

Amesema jeshi halipaswi kuvuruga mchakato wa kisiasa badala yake lihakikishe serikali na bunge la mpito vinalindwa na uchaguzi unafanyika kama ulivyopangwa.

Huku akitaka kuachiliwa haraka kwa viongozi wa mpito wanaoshikiliwa, Bwana Chungong amesema wananchi wa Burkina Faso wanataka utawala wa kidemokrasia na ni utashi wao unapaswa kuheshimiwa.