Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burkina Faso: Zeid alaani mapinduzi ya kijeshi

Burkina Faso: Zeid alaani mapinduzi ya kijeshi

Kufuatia jeshi huko Burkina Faso kutangaza mapinduzi, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu ndani ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na kitendo hicho.

Katika taarifa yake, Kamishna Zeid pamoja na kulaani amesema kitendo cha kushikiliwa kwa Rais wa mpito Michel Kafando na Waziri Mkuu Isaac Zida hakikubaliki.

Viongozi hao pamoja na mawaziri wengine wawili wanashikiliwa na askari wa jopo la ulinzi wa Rais kuanzia jana ambapo Kamishna Zeid ametaka waachiliwe mara moja katika mazingira ya utu na kibinadamu.

Halikadhalika amesihi viongozi wa mapinduzi hayo ya kijeshi kuepusha ghasia zozote zinazoweza kutokana na upinzani dhidi ya mapinduzi hayo ya kijeshi huku akitaka wazingatie haki ya wananchi kuandamana kwa amani.

Serikali ya mpito nchini Burkina Faso iliundwa mwaka jana kufuatia maandamano ya wananchi yaliyomlazimu Rais wa zamani wa nchi hiyo Blaise Compaore kukimbilia uhamishoni.

Uchaguzi ulitarajiwa kufanyika tarehe 11 mwezi ujao kuashiria mwisho wa kipindi cha mpito.