Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria yatia matumaini, lakini Afrika bado kuna kazi: Ripoti

Malaria yatia matumaini, lakini Afrika bado kuna kazi: Ripoti

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imesema lengo la kubadili mwelekeo wa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2015 limefanikiwa katika hali inayotia ushawishi mkubwa, ingawa bado mabilioni wako hatarini.

Ripoti hiyo ya shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na lile la afya WHO inazinduliwa Alhamisi ikiwa ni siku chache kabla ya kufikia ukomo malengo hayo ya maendeleo ya milenia, MDG na kuanza kwa malengo endelevu, SDG.

Akizungumzia ripoti hiyo kwa waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mkurugenzi wa programu ya malaria duniani kutoka WHO Dokta Pedro Alonso amesema hatua za kinga na tiba zimepunguza vifo kwa asilimia 60 tangu mwaka 2000 ikimaanisha kuokolewa kwa maisha Milioni 6.2 ambapo wengi wao ni watoto.

Dkt. Alonso amesema mafanikio hayo yanadhihirisha kuwa mikakati kama vile ongezeko la bajeti dhidi ya kudhibiti Malaria, matumizi ya vyandarua vyenye dawa, tiba sahihi, inafanya kazi ili kuondokana kabisa na ugonjwa huo unaoua watu Laki Nne kila mwaka akitaja eneo athirika zaidi..

(Sauti ya Alonso)

“Nchi 17 nyingi zao zikiwa bara Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zinahusika na asilimia 80 ya wagonjwa wote duniani na asilimia 78 ya vifo vyote.”

Hata hivyo amesema ili kuendeleza kasi ya sasa suala la msingi ni utekelezaji wa mwelekeko mpya wa kudhibiti ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 kwa hiyo..

(Sauti ya Dkt. Alonso)

“Tutahitaji kuwa tumechangisha karibu dola Bilioni Tisa au kama kwa umakini zaidi dola Bilioni Nane Nukta Saba ili kufanikisha harakati dhidi ya Malaria ifikapo mwaka 2030.”