Muarobaini wa ndoa utotoni Tanzania na Ethiopia wapatikana

Muarobaini wa ndoa utotoni Tanzania na Ethiopia wapatikana

Tanzania na Ethiopia zimefanikiwa katika kuepusha wasichana kuozwa na badala  yake wanaendelea na masomo kutokana na mikakati kadhaa iliyotumika ikiwemo kushirikisha jamii katika mijadala kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

Princess Mabel Van Oranje muasisi na mwenyekiti wa ubia wa kimataifa wa kumaliza ndoa za utotoni amesema hayo wakati wa mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuhusu harakati hizo.

Akinukuu ripoti ya baraza la idadi ya watu duniani, Princess Oranje ametaja mkakati mwingine kuwa ni ..

(Sauti ya Princess Mabel)

“Kuwapatia wasichana mbinu mbadala za kujiinua kiuchumi, kuhakikisha wana sare za shule na mahitaji yote ya shuleni, lakini pia mijadala hii ya kijamii imeleta tofauti kubwa.”

Akaenda mbali zaidi kutaja faida ya hatua hizo ambazo gharama yake kwa kila msichana ni dola 50 tu za kimarekani.

 (Sauti ya Princess Mabel)

“Na hebu fikiria tu manufaa ambayo msichana anapata kwa kuendelea kuwepo shule na kuwa na maisha yenye tija. Sote tunafahamu kuwa kuendelea kuwepo shule kila mwaka mmoja wa ziada shuleni unaongeza kipato chako kwa angalau asilimia 10.”

Katika utafiti huo baraza la idadi ya watu duniani lilibaini kuwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 17 ambao walipatiwa mbuzi ili wasiolewe na badala yake wasalie shuleni walikuwa na nafasi ya theluthi mbili zaidi kuendelea na masomo kuliko wale ambao hawakupatiwa miradi hiyo.