Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwaenzi wahanga kwa kuzuia daima majaribio ya nyuklia- Ban

Tuwaenzi wahanga kwa kuzuia daima majaribio ya nyuklia- Ban

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kuadhimisha Siku ya Kupinga Silaha za Nyuklia, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon, ametoa wito kwa nchi wanachama ziwaenzi wahanga wa majaribio ya zamani ya zana hizo kwa kuzuia majaribio kama hayo siku zijazo.

Bwana Ban ambaye amesema lengo la kutokomeza majaribio ya silaha za nyuklia limekuwa suala la kipaumbele katika kazi yake ya kidiplomasia, amesema amekutana na waathiriwa wa majaribio ya nyuklia na kujionea madhara ya kudumu ya majaribio hayo kwa jamii, mazingira na kiuchumi.

Katibu Mkuu amesema tangu jaribio la kwanza miaka 70 iliyopita katika jimbo la New Mexico, Marekani, kumekuwa na zaidi ya majaribio 2,000 ya silaha za nyuklia.

“Wengi hawakupata kupona kutokana na madhara ya majaribio ya silaha za nyuklia, yakiwemo sumu kwenye maji chini ya ardhi, saratani, watoto kuzaliwa na ulemavu na kuongezeka miyonzi ya nyuklia. Njia bora ya kuwaenzi wahanga wa majaribio ya zamani ni kuzuia majaribio siku zijazo.”

Ban amesema siku ya kupinga silaha za nyuklia, ambayo huadhimishwa Agosti 29, ni ya kutuma ujumbe thabiti kwamba jamii ya kimataifa imeshikamana kuchukua hatua itakayoleta ulimwengu salama zaidi, usio na silaha za nyuklia.