Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la milenia kuhusu matibabu dhidi ya HIV limetimizwa- UNAIDS

Lengo la milenia kuhusu matibabu dhidi ya HIV limetimizwa- UNAIDS

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya HIV na Ukimwi, UNAIDS, limetangaza leo kuwa lengo la milenia la kuhakikisha kuwa watu milioni 15 wanapata matibabu ya dawa kupunguza makali ya HIV ifikapo mwaka 2015, limetimizwa n ahata kuzidishwa, miezi tisa kabla tarehe ya ukomo wa malengo ya milenia.Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Maambukizi mapya ya HIV yamepungua kwa asilimia 35, na vifo vitokanavyo na Ukimwi kupungua kwa asilimia 41.

Jitihada za kimataifa dhidi ya HIV zimeepusha maambukizi mapya milioni 30, na takriban vifo milioni 8 vitokanavyo na Ukimwi tangu mwaka 2000, malengo ya milenia yalipowekwa.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa kongamano la tatu kuhusu Ufadhili kwa Maendeleo, imebainisha kuwa kukabiliana na HIV kumekuwa moja ya uwekezaji wenye busara zaidi katika afya ya kimataifa na maendeleo, ikiwa na  matokeo yanayoweza kupimwa, kwa watu na kwa uchumi. Wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema …

Ulimwengu umefanikiwa katika kusitisha na kubadili mwelekeo wa mlipuko wa Ukimwi. Sasa ni wakati wa kuahidi kutokomeza Ukimwi kama sehemu ya malengo ya maendeleo endelevu.”

Ripoti pia inaonyesha kuwa ulimwengu upo kwenye mkondo sahihi wa kutimiza lengo la kuwekeza dola bilioni 22 katika jitihada za kupambana na Ukimwi ifikapo mwaka 2015, na kwamba juhudi za kina katika miaka mitano ijayo zinaweza kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.