Uwekezaji haba katika afya ya akili ni lazima ubadilishwe kimataifa- WHO
Matatizo ya afya ya akili huathiri nchi zote, zikiwemo tajiri na maskini, lakini malengo yanayodhamiria kuwasaidia wahitaji bado yapo mbali sana kutimizwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO.
Ikitoa mfano wa kutokuwepo usawa katika utoaji wa huduma kwa wenye matatizo ya afya ya akili, WHO imesema baadhi ya sababu ya hali hii ni unyanyapaa na kutojua cha kufanya kuhusu matatizo ya afya ya akili.
Ramani ya WHO kuhusu afya ya akili mwaka 2014 inaonyesha kuwa hakuna nchi inayofanya kila inachopaswa kufanya kukabiliana na mzigo unaozidi kuwa mkubwa wa afya ya akili, na kwingineko, haki za binadamu za waathiriwa zimo hatarini.
WHO imesema ni asilimia 1 tu wataalam wa afya ndio wanaofanya kazi katika sekta ya afya ya akili, ikiongeza kuwa kimataifa, kuna mhudumu mmoja tu wa afya ya akili kwa kila watu 10,000.
Kuna pia tofauti kubwa kwa kiasi cha fedha kinachotumiwa kwa waathiriwa, kulingana na mahali walipo duniani, kwa mujibu wa afisa wa WHO, Shekhar Saxena
“Tunajua kuwa nchi za kipato cha chini na cha wastani zina rasilmali chache kwa ujumla. Lakini tofauti ni kubwa mno, wakati mwingine hata rasilmali za nchi tajiri ni mara mia moja zaidi kuliko zile za nchi za kipato cha chini na wastani. Mzigo katika nchi za kipato cha chini na wastani bado ni mkubwa sana. Kwa hiyo hakuna sababu ya nchi hizo kuwekeza rasilmali chache sana katika afya ya akili kutoka kwa bajeti zao za jumla za afya.”
WHO imesema, hata katika nchi tajiri ambazo zinatarajiwa kuwekeza zaidi katika afya ya akili, ni watu wachache sana ambao wanapata huduma wanazohitaji.