Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza katika kilimo endelevu ni ufunguo wa maendeleo

Kuwekeza katika kilimo endelevu ni ufunguo wa maendeleo

Shirika la kimataifa la maendeleo ya kilimo, IFAD, limesema ufadhili zaidi unahitajika ili kuendeleza kilimo endelevu, kwa sababu asilimia 78 ya watu wanaokumbwa na ukosefu wa uhakika wa chakula wanaishi mashambani.Katika kutambua hilo, IFAD katika kuelekea kongamano la kimataifa kuhusu ufadhili kwa maendeleo mjini Addis Ababa, Ethiopia, imeunda chanzo kipya cha ufadhili kupitia mikopo, uitwao sovereign borrowing framework, ambao utaliwezesha shirika hilo kukopa dola milioni 500 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kusaidia watu zaidi ya milioni 100.

Akihojiwa na idhaa hii, Mohamed Beavogui, mkurugenzi wa idara ya uhisani ya IFAD, amesema kulenga wakulima wadogo na maskini ni lazima ili kutokomeza umaskini ifikapo 2030,

"Inamaanisha kuwekeza katika maeneo ya mashambani, kuwekeza kupitia ufadhili, sera, kujenga mamlaka bora, ili kubadili maeneo hayo, ili yavutie vijana, ili kutunza mazingira yetu, ili tofauti za kiuchumi zitokomezwe na jamii jumuishi iwe kipaumbele".  

Bwana Beavogui amesisitiza kwamba maendeleo endelevu si pesa tu, bali pia kuwekeza katika watu, elimu na sera, akitaja mfano wa miradi ya IFAD iliyfanyikiwa kuwezesha wanawake kumiliki ardhi nchini Ethiopia.