Uwekezaji unaolenga wanawake unahitajika ili kuimarisha usawa wa kijinsia

Uwekezaji unaolenga wanawake unahitajika ili kuimarisha usawa wa kijinsia

Uwekezaji unaolenga wanawake ndio njia pekee ya kukabiliana na tofauti za usawa wa kijinsia na ubaguzi  na kuleta mabadiliko thabiti. Hiyo ni kauli ya Naibu Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Umoja wa Matifa linalohusika na maswala ya wanawake Lakshmi Puri alipozungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa  kama inavyoelezea taarifa ya Grace  Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Bi. Puri amesema kwamba kwa sasa kuna pengo la uwekezaji katika maswala ya wanawake ikiwemo katika sekta ya elimu, afya, usafiri, nyumba, sheria na  taasisi na huduma ambazo zinawalenga wanawake, akisema inamaanisha kwamba wanawake wanapaswa kuwezeshwa kupitia uwekezaji.

Amesema swala la uwekezaji kwa wanawake halijawahi kupewa kipaumbele kwa sababu……

“Inachukuliwa kama jambo la baadaye, kuna tofauti kubwa ya maswala ya kijinsia na ubaguzi ambayo inahitaji kutatuliwa ili kuleta usawa na hiyo inahitaji uwekezaji. Kuna makadirio kwamba lengo la tatu linaloangazia maswala ya usawa wa kijinsia na uimarishaji wa wanawake lilikuwa na pengo la ufadhili la dola biloni 83 katika nchi maskini. Kwa sasa kuna uwekezaji mdogo ambapo tunapaswa kuziba pengo la raslimali”

Kuelekea mkutano wa kimataifa wa ufadhili kwa maendeleo nchini Ethiopia Bi. Puri amesema wana matumaini kwamba kutakuwa na makubaliano ambayo yatawiana na ajenda ya maendeleo endelevu baada ya  mwaka 2015.