Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Nigeria yaombwa kuheshimu haki za binadamu ikipambana na Boko Haram

Serikali ya Nigeria yaombwa kuheshimu haki za binadamu ikipambana na Boko Haram

Kikao cha 29 cha Baraza la Haki za Binadamu kikiendelea mjini Geneva, Uswisi, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema ni lazima serikali ya Nigeria iheshimu haki za binadamu wakati wa kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Katika hotuba yake, Kamishna Zeid amekaribisha hatua zilizochukuliwa na serikali ya Nigeria ili kudhibiti baadhi ya maeneo ya Nigeria ambayo yaliathiriwa na mashambulizi ya Boko Haram, huku akieleza wasiwasi wake kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaoripotiwa kutekelezwa na wanajeshi wa serikali.

Halikadhalika amesema uhalifu uliotekelezwa na Boko Haram umesababisha mateso na mzozo wa kiuchumi na wa kibinadamu kwani waasi wameteketeza miundumbinu, vituo vya afya, na mashamba.

Juu ya hayo, amemulika hali ya wanawake na wasichana waliotiwa ujauzito kwa kubakwa na waasi wa Boko Haram, akisema wangepaswa kuruhusiwa kutoa mimba hizo kiusalama, akisisitiza kwa ujumla umuhimu wa suluhu ya kisiasa.

Wakati ambapo serikali ya Nigeria na nguvu za kijeshi za kikanda zinaendelea kukomboa maeneo, naamini muda umefika kutambua kwamba suluhu ya kisiasa linahitajika, pamoja na uwajibikaji, maridhiano na hatua za kuimarisha haki za kijamii na kiuchumi, na utawala bora. Kuaminiana kunapaswa kujengwa upya, hasa baina ya mamlaka za serikali na jamii.”