Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na msimamo wa Burundi kufanya uchaguzi Juni 29.

Ban asikitishwa na msimamo wa Burundi kufanya uchaguzi Juni 29.

Katibu Mkuu ameelezea kusikitishwa  kwake na serikali ya Burundi kusisitiza kufanya uchaguzi Juni 29 licha ya ukosefu wa usalama wa kisiasa na kuendelea.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu iliyotolewa jumapili mjini New York, inasema wakati timu ya kimataifa ya uwezeshaji upatanisho ikifanya kazi kusaidia pande nchini Burundi kufikia makubaliano ili kufanyika uchaguzi huru, wa haki, jumuishi na wa amani, Ban anasononeshwa na misisamo ya pande husika ambayo husababisha juhudi hizo muhimu kutokuwa jumuishi.  

Amesisitiza wito wa uamuzi baraza la usalama ikiwamo azimio namba 2137 la mwaka 2014 ambalo limetoa mamlaka kwa ujumbe wa uangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi (MENUB) kuangalia zoezi  la uchaguzi na kusema kuwa MENUB utaendelea  kufanya kazi hiyo kwa taaluma bila kuegemea upande wowote kulingana na sheria za kitaifa zinazohusika na masula ya uchaguzi na vyombo vya kimataifa, kanuni, na sheria za uangalizi wa uchaguzi.

Katibu Mkuu amefafanua jukumu la serikali ya Burundi la kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya usalama na pia kuhakikisha usalama wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa ili wafanye kazi zao walizoagizwa kwa uhuru bila vitisho au unyanyasaji.

Bwana Ban kadhalika amerejelea wito wake kwa viongozi wote wa kisiasa wa Burundi kuzingatia maslahi ya watu wa nchi yao na kusuluhisha masuala ya kisiasa kupitia majadiliano ili kuhifadhi amani na kuwezesha mshikamano wa kitaifa.

Akilaani mashambulizi ya siku za hivi karibuni yaliyoripotiwa nchini humo ametaka raia wote kujizuia dhidi ya machafuko kwa mujibu wa mkataba wa kupinga machafuko uliokubaliwa na pande zote.