Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akumbuka watendaji wanaoelimisha umma dhidi ya mateso akitaka walindwe

Ban akumbuka watendaji wanaoelimisha umma dhidi ya mateso akitaka walindwe

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kusaidia wahanga waliokumbwa na mateso, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametumia ujumbe wake kusaka mshikamano na watetezi wa haki za binadamu ambao licha ya ujasiri wao wanakabiliwa na mateso.

Amesema watetezi  hao wanaweka maisha yao rehani kwa lengo la kuelimisha watu juu ya haki zao dhidi ya mateso akitolea mfano wanasheria, madaktari na watendaji wa kijamii.

Ban amesema watu hao wanahaha kutwa kucha kuhakikisha watu waliopata mateso wanaibuka washindi na wanaweza kujumuika tena kwenye jamii yao.

Kwa mantiki hiyo ametaja serikali kukumbuka wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kuhusu usaidizi wa wahanga hao akisema Umoja wa Mataifa kupitia mfuko wake maalum unatoa fedha kwa ajili ya vituo vya urejeshaji watu katika maisha ya kawaida, pamoja na hospitali, vituo vya wakimbizi na maeneo mengine mengi.

Ametoa wito kwa nchi wanachama na wahisani binafsi kuchangia mfuko huo kupitia tovuti http://donatenow.ohchr.org/torture/ huku akitaka nchi ambazo hazijatia saini mkataba wa kimataifa dhidi ya mateso kufanya hivyo hima bila kuchelewa