Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya dawa za kulevya hayajapungua - Ripoti ya UNODC

Matumizi ya dawa za kulevya hayajapungua - Ripoti ya UNODC

Matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa imara kote duniani, kulingana na ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na dawa na uhalifu, UNODC, ambayo imezinduliwa leo, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya kupinga matumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, inakadiriwa kuwa jumla ya watu milioni 246, ikiwa ni asilimia 5 ya watu wenye umri wa miaka kati ya 15 na 64 kote duniani, walitumia aina fulani ya dawa ya kulevya mnamo mwaka 2013.

Watu milioni 27 wana tatizo la uraibu wa kutumia dawa za kulevya, nusu yao wakitumia zile za kudunga sindano.

Akiizindua ripoti hiyo hapa kwenye Umoja wa Mataifa, Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson amesema..

“Ripoti hii inaweka msingi wa kupambana na tatizo ambalo linakwamisha jamii na afya ya mamilioni ya watu duniani. Changamoto ni nyingi. Uhusiano kati ya uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, ugaidi na ukatili wa silaha unaongezeka, ukiwa na athari nyingi mbaya za kiusalama, utawala na maendeleo, bila kutaja madhara yake kwa watu na jamii.”

Ripoti pia imezinduliwa mjini Geneva na Vienna, ambako Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Yury Fedotov amesema kuwa ingawa matumizi ya dawa za kulevya yamebaki imara, ni mtu mmoja tu kati ya watu sita wenye tatizo la uraibu ndiye anayepata matibabu.