Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP yasaidia zaidi ya nchi 30 kushiriki kwenye makubaliano ya tabianchi

UNDP yasaidia zaidi ya nchi 30 kushiriki kwenye makubaliano ya tabianchi

Wataalam wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, wameeleza kuwa na matumaini makubwa kuhusu mwelekeo wa mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Jo Scheuer na Cassie Flynn, watalaam wa UNDP kuhusu maswala ya mabadiliko ya tabianchi wamezungumza leo na waandishi wa habari mjini New York Marekani kuhusu matokeo ya mkutano uliofanyika mjini Bonn, Ugerumani, kwanzia tarehe Mosi Juni hadi tarehe 11 ili kuandaa kongamano la Paris la Disemba mwaka huu kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP21.

Wamesema kwamba kazi kubwa iliyofanyika ni kukusanya michango ya nchi wanachama katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi, tayari nchi 38 zikiwa zimetangaza michango yao.

Aidha Jo Sheuer ameeleza kwamba UNDP inasaidia zaidi ya nchi 30 duniani kote ili kutayarisha michango yao kwa ajili ya kongamano la Paris, akizingatia lengo la kongamano hilo muhimu :

"Msimamo wetu ni kuhakikisha kwamba tunatimiza matarajio ya Paris, na kwamba tunatekeleza yanapotakiwa. Tunapaswa kukumbuka kwamba Paris si kongamano tu, kila mtu atafurahi kwenda Paris, si kitu kibaya, lakini ni kuangalia tunafanya nini kama jamii ya kimataifa ili kukabiliana na changamoto hizo katika miongo kadhaa ijayo na kuhakikisha mabadiliko ya tabianchi hayaondoi maendeleo, hayapunguzi ukuaji wa uchumi na hayazidishi umaskini."

Kongamano la Kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi litakalofanyika mjini Paris, Ufaransa mwezi Disemba mwaka huu, linatarajia kufikia makubaliano ya kimataifa ili kuhakikisha ongezeko la joto duniani halizidi nyuzi mbili za selisyasi.