Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wana haki ya kulindwa shuleni, nyumbani na katika jamii- Ban

Watoto wana haki ya kulindwa shuleni, nyumbani na katika jamii- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa watoto wana haki ya kupewa ulinzi shuleni, nyumbani na katika jamii, wakati akilihutubia Baraza la Usalama leo katika mjadala wa wazi kuhusu watoto na migogoro ya silaha.

Ban amesema haki za watoto zinapaswa kupewa kipaumbele katika juhudi za kujenga mustakhbali wenye utu kwa wote.

Akizungumza kuhusu ripoti mpya kuhusu watoto katika mizozo ambayo imezua utata miongoni mwa nchi wanachama, Ban amesema ripoti hiyo inabainisha uhalifu mkubwa uliotendwa dhidi ya watoto mwaka 2014, na kwamba matakwa ya kitaifa yasighubike lengo la ripoti hiyo, ambalo ni kuwalinda watoto..

“Hili ni suala la lazima kimaadili na wajibu wa kisheria. Wale wanaotekeleza vitendo vya kijeshi vinavyosababisha ukiukaji mwingi wa haki za watoto, watamulikwa, bila kujali kinachowavutia kufanya hivyo. Nchi wanachama zinapaswa kutafuta njia zote za kuwalinda watoto wanaoathiriwa na mzozo.”

Ban amesema njia moja ya kuwalinda watoto, ni kumaliza ukwepaji sheria wa wale wanaotenda uhalifu dhidi ya watoto.