Skip to main content

Kampeni ya chanjo ya polio inayovuka mipaka yatekelezwa Nigeria

Kampeni ya chanjo ya polio inayovuka mipaka yatekelezwa Nigeria

Nchini Nigeria, watoto wapatao 25,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wamepewa chanjo dhidi ya polio katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo mpakani na Niger.

Taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Afya Duniani WHO inasema kwama jamii zinazoishi kwenye maeneo ya mpakani ziko hatarini kuambukizwa na kirusi cha polio, huku baadhi ya visa vikiripotiwa kwenye majimbo ya kaskazini mwa nchi mwaka 2012 na 2014.

Watendaji wa WHO wamesambazwa kwenye barabara zote za kuingia nchini Nigeria, hadi zile zinazopita porini ambapo watoto wote waliokuwa wakivuka mpaka wakisimamiwa na kupewa chanjo.

Kampeni hiyo imetekeleza kwa ushirikiano na viongozi wa jamii kwa pande zote mbili za mpaka.

WHO inasema ufuatiliaji utaendelea ili kubaini visa vya polio, na mikutano ya kila mwezi inatarajiwa kufanyika na wadau wa Nigeria, Niger na Cameroon ili kubaini changamoto zilizopo na mafanikio yaliyopatikana.