Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha Bonn kuimarisha harakati za UM: Ban

Kituo cha Bonn kuimarisha harakati za UM: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema atatumia mkutano wa kesho na viongozi wa nchi Saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 kuwasihi watimize wajibu wao wa kisiasa na kimaadili ili kufanikisha malengo endelevu ulimwenguni.

Ban amesema hayo huko Bonn Ujerumani wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa jengo la kituo cha kimataifa cha mkutano lililofanyiwa upanuzi.

Amesema dunia sasa inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, mizozo ya kisiasa kama vile Syria na Yemen akisema mwaka 2015 ni mwaka wa dunia ikiwemo viongozi hao, kuchukua hatua kwa dunia iwe sehemu ya amani, na maendeleo endelevu sawia.

Sanjari na viongozi hao, amesema kituo hicho kitakuwa fursa ya mikutano kwa kuwa mara nyingi maeneo ya kimataifa ya kufanyia mashaurino yanatingwa na nafasi na hivyo ni wakati muafaka kwa mashauriano thabiti kwa mustakhbali bora wa dunia.

Ameshukuru serikali ya Ujerumani kwa mchango wake katika upanui huo sambamba na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Bonn.

Katika hatua nyingine Bwana Ban amekuwa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ambapo wamejadili mabadiliko ya tabianchi, maendeleo endelevu na mzozo wa Ukraine na Gaza na suala la wahamiaji.